Matthew 12:1-14

Bwana Wa Sabato

(Marko 2:23-28; Luka 6:1-5)

1 aWakati huo Yesu alipitia kwenye mashamba ya nafaka siku ya Sabato. Wanafunzi wake walikuwa na njaa, nao wakaanza kuvunja masuke ya nafaka na kuyala. 2 bLakini Mafarisayo walipoona jambo hili, wakamwambia, “Tazama! Wanafunzi wako wanafanya jambo lisilo halali kufanywa siku ya Sabato.”

3 cYesu akawajibu, “Je, hamjasoma alichofanya Daudi na wenzake walipokuwa na njaa? 4 dAliingia katika nyumba ya Mungu, akala mikate iliyowekwa wakfu, yeye na wenzake, jambo ambalo halikuwa halali kwao kufanya, isipokuwa makuhani peke yao. 5 eAu hamjasoma katika Sheria kwamba siku ya Sabato makuhani huvunja sheria ya Sabato Hekaluni lakini hawahesabiwi kuwa na hatia? 6 fNawaambia wazi kwamba, yeye aliye mkuu kuliko Hekalu yupo hapa. 7 gKama mngekuwa mmejua maana ya maneno haya, ‘Nataka rehema, wala si dhabihu,’ msingewalaumu watu wasio na hatia, 8 hkwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

Yesu Anamponya Mtu Aliyepooza Mkono

(Marko 3:1-6; Luka 6:6-11)

9 iYesu akaondoka mahali hapo, akaingia ndani ya sinagogi lao, 10 jna huko alikuwepo mtu aliyepooza mkono. Wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu, wakamuuliza, “Je, ni halali kuponya siku ya Sabato?”

11 kYesu akawaambia, “Ni nani miongoni mwenu, mwenye kondoo wake ambaye huyo kondoo akitumbukia shimoni siku ya Sabato hatamtoa? 12 lMtu ana thamani kubwa kuliko kondoo. Kwa hiyo ni halali kutenda mema siku ya Sabato.”

13Ndipo akamwambia yule mtu, “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukaponywa ukawa mzima kama ule mwingine. 14 mLakini Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri baya juu ya Yesu jinsi watakavyoweza kumuua.

Copyright information for SwhNEN